
Ziara ya Merkel mjini Moscow inakuja wakati Kansela huyo akikaribia mwisho wa uongozi wake wa karibu miaka 16 wa Ujerumani. Yeye na Putin, ambaye amehudumu kama rais wa Urusi au waziri mkuu tangu 2000, walimudu kuweka mawasiliano ya mara kwa mara kwa miaka mingi licha ya tofauti zao nyingi za kisiasa.
Hata hivyo, uhusiano wa kibinafsi kati ya viongozi hao umezorota tangu 2014, wakati Urusi ilipochukua kwa nguvu Rasi ya Crimea nchini Urusi na kuwaunga mkono waasi wanaopigania kujitenga mashariki mwa Ukraine, na pia vitendo vingine vya kimabavu vya Moscow.
Mwaka 2002, Merkel alikuwa kiongozi wa kilichokuwa wakati huo chama cha upinzani cha Christian Democratic Union (CDU). Putin alikuwa wakati huo rais mpya wa Urusi. Baada ya kukutana na Putin nchini Urusi, Merkel aliwaambia wasaidizi wake kwa utani kwamba amefaulu "mtihani wa KGB" kwani aliweza kutuliziana macho na Putin.
Wachambuzi hata hivyo wana mashaka kama mkutano wa Merkel na Putin utaimarisha mahusiano ya Ujerumani na Urusi.
Mchambuzi wa kisiasa kutoka Baraza la Ujerumani kuhusu Mahusiano ya Kigeni Stefan Meister anasema Urusi imekuwa utawala wa kimabavu. Na kuzorota kwa mahusiano kati ya nchi hizo kunadhihirishwa katika kuharibika kwa uhusiano wa kibinafsi wa viongozi hao wa muda mrefu. "Kimsingi, mahusiano kati ya Ujerumani na Urusi yamezorota kabisa. Yanaharibika kila mwaka. Merkel hatoweza kushawishi lolote katika mazungumzo hayo. Lakini bila shaka atajadili masuala haya, Nord Stream 2, Donbas, masuala ya usalama Afghanistan. Na huo ndio utakuwa urithi wake."
Msemaji wa Merkel, Steffen Seibert aliwaambia waandishi wa habari wiki hii mjini Berlin, kuwa mazungumzo ya leo mjini Moscow yatakuzwa kuhusu maswali makubwa ya kimataifa yanayostahili majibu.
Kansela Merkel ameelekea Urusi katika mkesha wa kumbukumbu ya Navalny kuanza kuugua ghafla wakati akiwa kwenye ndege katika mkoa wa Siberia mnamo Agosti 20, 2020. Kiongozi huyo wa upinzani akahamishiwa Ujerumani kwa matibabu maalum. Madaktari waligundua aliwekewa sumu ya kuuwa mishipa ya fahamu iliyotengenezwa na Wasovieti.
Merkel mwenye umri wa miaka 67, ambaye alikulia katika upande wa Kikomunisti wa iliyokuwa Ujerumani Mashariki na kuzungumza vizuri Kirusi, kila mara anasisitiza kuwa mahusiano na Urusi yanaweza tu kuimarika kupitia mazungumzo. Ziara yake itakuwa moja ya safari za mwisho za kigeni akiwa Kansela kwa vile hatogombea uchaguzi wa Ujerumani mwezi ujao.
Putin mwenye umri wa miaka 68, ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 20, ndiye kiongozi aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi Urusi tangu dikteta wa Kisovieti Josef Stalin.

0 Comments