Na Mwandishi Wetu,
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ni miongoni mwa Taasisi za
mwanzo kujiunga na Mfumo wa Utoaji Huduma wa Pamoja wa Serikali (One Stop Service Centre) ambao Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ameuzindua leo Septemba 6, 2021 jijini Dar es Salaam.
WAZIRI Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, amezitaka Taasisi nyingine za Serikali ambazo bado
hazijajiunga na Mfumo huo unaoratibiwa na Shirika la Posta Nchini, kuhakikisha zinajiunga
ndani ya mwaka huu wa fedha wa 2021/2022.
“Mradi huu unaenda kubadilisha namna ya utoaji huduma bora, ni muhimu kuharakisha na kuhakikisha kwamba unafanikiwa, hivyo basi nazielekeza taasisi zote zinazotoa huduma kuongeza kasi ya kujiunga na Utaratibu wa Utoaji Huduma wa Pamoja.”Alisisitiza.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine Ndungulile amezitaja
Taasisi ambazo tayari zimeanza kutoa huduma kupitia mfumo huo kuwa ni pamoja na
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Vizazi na Vifo (RITA), Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa
Umma (PSSSF), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Idara ya Uhamiaji,
BRELA, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NHIF) na benki ya CRDB.
Kwa kuanzia Mfumo huo tayari umezinduliwa kwenye mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam
na kwamba lengo ni kufikia mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani, alifafanua
Dkt. Ndungulile.
Akizungumza pembezoni mwa hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), C.P.A Hosea Kashimba alisema, Taasisi yake iliamua kujiunga mara moja na Mfumo huo kwa sababu Mfuko unawajali Wanachama na Wateja
wake.
“Tumeona utaratibu huu ni mzuri, utapelekea kumuhudumia mwanachama kwa haraka lakini pia kuondoa usumbufu ambao pengine mwanachama anaweza kukutana nao hivyo anaweza akafika hapa na kuhudumiwa na kama kuna taarifa zinahitajika kutoka Taasisi nyingine
Taasisi hizo nyingine ziko hapa ikiwemo NIDA, RITA na Taasisi ambazo tunashirikiana katika kutoa huduma.” Alifafanua C.P.A Kashimba.
WAZIRI Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa (kulia) akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) C.P.A Hosea Kashimba(Kushoto). wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Pamoja wa Utoaji Huduma Taasisi za Umma unaoratibia na Shirika la Posta nchini. Uzinduzi huo ulifanywa na Waziri Mkuu Septemba 6, 2021 jijini Dar es Salaam.

Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Bw. Macrice Daniel Mbodo
0 Comments